Micah 4

Mlima Wa Bwana

(Isaya 2:2-4)

1 aKatika siku za mwisho mlima wa Hekalu la Bwana utaimarishwa
kama mlima mkuu miongoni mwa milima yote;
utainuliwa juu ya vilima,
na watu wa mataifa watamiminika humo.

2 bMataifa mengi yatakuja na kusema, “Njooni, twendeni mlimani mwa Bwana,
kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo.
Atatufundisha njia zake,
ili tuweze kuenenda katika mapito yake.”
Sheria itatoka Sayuni,
neno la Bwana litatoka Yerusalemu.

3 cAtahukumu kati ya mataifa mengi,
na ataamua migogoro ya mataifa
yenye nguvu na yaliyo mbali.
Watafua panga zao ziwe majembe,
na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi.
Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine,
wala hawatajifunza vita tena.

4 dKila mtu ataketi chini ya mzabibu wake
na chini ya mtini wake,
wala hakuna mtu atakayewaogopesha,
kwa kuwa Bwana Mwenye Nguvu Zote amesema.

5 eMataifa yote yanaweza kutembea
katika jina la miungu yao;
sisi tutatembea katika jina la Bwana
Mungu wetu milele na milele.

Mpango Wa Bwana

6 f“Katika siku hiyo,” asema Bwana, “nitawakusanya walemavu;
nitawakusanya walio uhamishoni
na wale niliowahuzunisha.

7 gNitawafanya walemavu kuwa mabaki,
wale waliofukuzwa kuwa taifa lenye nguvu.
Bwana atatawala juu yao katika Mlima Sayuni
kuanzia siku hiyo na hata milele.

8 hLakini kuhusu wewe, ee mnara wa ulinzi wa kundi,
ee ngome ya Binti Sayuni,
milki ya awali itarudishwa kwako,
ufalme utakuja kwa Binti Yerusalemu.”


9 iKwa nini sasa unalia kwa nguvu:
kwani huna mfalme?
Je, mshauri wako amekufa, hata maumivu yakukamate
kama ya mwanamke
aliye na utungu wa kuzaa?

10 jGaagaa kwa utungu, ee Binti Sayuni,
kama mwanamke mwenye utungu wa kuzaa,
kwa kuwa sasa ni lazima uuache mji
ukapige kambi uwanjani.
Utakwenda Babeli;
huko utaokolewa.
Huko Bwana atakukomboa
kutoka mikononi mwa adui zako.


11 kLakini sasa mataifa mengi
yamekusanyika dhidi yako.
Wanasema, “Mwache anajisiwe,
macho yetu na yatazame Sayuni kwa furaha!”

12 lLakini hawayajui
mawazo ya Bwana;
hawauelewi mpango wake,
yeye awakusanyaye kama miganda
kwenye sakafu ya kupuria.


13 m“Inuka upure, ee Binti Sayuni,
kwa kuwa nitakupa pembe za chuma;
nitakupa kwato za shaba
na utavunja vipande vipande mataifa mengi.”

Utatoa mapato yao waliopata kwa udanganyifu kwa Bwana,
utajiri wao kwa Bwana wa dunia yote.
Copyright information for SwhKC